1 Corinthians 12

1Kuhusu karama za rohoni, kaka na dada zangu sitaki mkose kufahamu. 2Mwajua ya kuwa mlipokuwa wapagani mliongozwa kufuata sanamu zisizoongea, kwa njia zozote mliongozwa nazo. 3Kwa hiyo, nataka mfahamu kwamba hakuna yeyote anenaye kwa Roho wa Mungu akisema, “Yesu amelaaniwa.” Hakuna yeyote atakayesema, “Yesu ni Bwana,” isipokuwa katika Roho Mtakatifu.

4Basi kuna karama tofauti tofauti, bali Roho ni yeye yule. 5Na kuna huduma tofauti tofauti, bali Bwana ni yeye yule. 6Na kuna aina mbalimbali za kazi, lakini Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.

7Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. 8Maana mtu mmoja amepewa na Roho neno la hekima, na mwingine neno la maarifa kwa Roho yule yule.

9Kwa mwingine humpa imani kwa Roho yeye yule, na kwa mwingine karama ya uponyaji kwa Roho mmoja. 10Kwa mwingine matendo ya nguvu, na mwingine unabii. Na kwa mwingine uwezo wa kupambanua roho, mwingine aina mbalimbali za lugha, na kwa mwingnine tafsiri za lugha. 11Lakini Roho ni yule yule atendaye kazi hizi zote, kumpa kila mtu karama kwa kadiri ya uchaguzi wake mwenyewe.

12Kwa maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote ni vya mwili ule ule, vivyo hivyo na Kristo. 13Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi au Wayunani, kwamba tu watumwa au huru, na wote tulinyweshwa Roho mmoja.

14Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. 15Ikiwa mguu utasema, “kwa kuwa mimi si mkono, mimi si sehemu ya mwili,” hiyo haiufanyi kutokuwa sehemu ya mwili. 16Na ikiwa sikio litasema, “kwa kuwa mimi si jicho, mimi si sehemu ya mwili,” hiyo hailifanyi kutokuwa sehemu ya mwili. 17Kama mwili wote utakuwa jicho, kungekuwa wapi kusikia? Kama mwili wote ukiwa sikio, kungekuwa wapi kunusa?

18Lakini Mungu aliweka kila kiungo cha mwili mahali pake kama alivyopanga mwenyewe. 19Na kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? 20Hivyo sasa viungo ni vingi, lakini mwili ni mmoja.

21Jicho haliwezi kuuambia mkono, “sina haja na wewe.” Wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu, sina haja na ninyi.” 22Lakini viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa na heshima kidogo vyahitajika zaidi. 23Na viungo vya mwili tunavyodhani vina heshima kidogo, twavipa heshima zaidi, na viungo vyetu visivyo na mvuto vina uzuri zaidi. 24Na sasa viungo vyetu vilivyo na mvuto havina haja ya kupewa heshima, kwa kuwa tayari vina heshima. Lakini Mungu ameviunganisha viungo vyote pamoja, na amevipa heshima zaidi vile visivyo heshimiwa.

25Alifanya hivyo ili pasiwepo mgawanyiko katika mwili, bali viungo vyote vitunzane kwa upendo wa mmoja. 26Na wakati kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote vyaumia kwa pamoja. Au wakati kiungo kimoja kikiheshimiwa, viungo vyote vifurahi kwa pamoja. 27Sasa ninyi ni mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.

28Na Mungu ameweka katika kanisa kwanza mitume, pili manabii, tatu waalimu, kisha wale wote watendao matendo makuu, kisha karama za uponyaji, wale wasaidiao, wale wafanyao kazi ya kuongoza, na wote walio na aina mbalimbali za lugha. 29Je sisi sote ni mitume? Sisi sote ni manabii? Sisi sote ni waalimu? Je sisi sote tunafanya matendo ya miujiza?

30Je sisi sote tuna karama ya uponyaji? Sisi sote tunaongea kwa lugha? Sisi sote tunatafsiri lugha? Tafuteni sana karama zilizo kuu. Nami nitawaonesha njia iliyo bora zaidi.

31

Copyright information for SwaULB